HITAJI LA MATUMAINI LINAMEA.

Mwaka 2010 aliyekuwa Askofu mstaafu wa kanisa la kilutheri Tanzania (ELCT), marehemu Ambilikile Mwasapile alitangaza kuwepo kwa dawa inayotibu magonjwa yote ikiwamo magonjwa sugu kama Kisukari, Kansa na Kifua kikuu dawa ambayo kwa mujibu wa maelezo yake ilitokana na maono ya ndoto aliyooteshwa na Mungu. Mwasapile alituhumu pia dawa hiyo kutibu maambukizi ya virusi wanaosababisha kushuka kwa kinga (Ukimwi).


Babu (kama alivyofahamika na wengi) alitembelewa na watu wa kila rika, na jinsia, viongozi wa serikali, taasisi na vitengo binafsi, masikini na matajiri, na wote walimiminika kuungana na mamilioni ya Watanzania waliokata tamaa kwa kuelemewa na maradhi. Kama haitoshi maelfu wengine kutoka nchi jirani pia walifurika kwenye mji wa Loliondo jijini Arusha ambako ndiko yalikuwako makazi ya Askofu kwa muda huo, kwenda kujipatia dawa hiyo.

Miongoni mwa waliokuwepo kwenye umati huo alikuwamo Mama U (si jina halisi nikikusudia kuficha utambulisho) aliyesafiri kwa zaidi ya kilometa 600 kutoka Dar es salaam kufuata bidhaa hii adhimu ya matumaini. Mama U alikuwa mwathirika wa virusi vinavyosababisha Ukimwi na alikuwa anatumia dawa za kupunguza makali ya virusi hao za ARVs kwa zaidi ya miaka mitano. Aliungana na mamia ya majirani wa mtaani kwake kwenda Loliondo. Alifunga biashara yake ya mgahawa kwa muda, akachukua pesa zake za akiba kwenda kushiriki uponyaji.

Alikaa huko kwa wiki moja na siku kadhaa kusubiri zamu yake kwani umati ulikuwa mkubwa mno. Mamia kwa mamia walikosa dawa na kwa mujibu wa ripoti kadhaa, wagonjwa wengine walifariki kabla hata ya kufika nyumbani kwa Babu. Hali ya miundombinu muhimu kama usafiri, malazi na upatikanaji wa chakula na maji safi haikulingana na idadi ya ghafla ya watu waliofika kwenye mji huo kupata dawa, lakini kwa babhati nzuri Mama U alikuwa miongoni mwa wachache waliofanikiawa kupata dawa na alirudi Dar es salaam kuanza maisha mapya akiwa na tumaini la uponyaji.

MAISHA MAPYA, TUMAINI JIPYA

Mama U alikuwa na nuru usoni, afya mwilini, pia matumaini kichwani kiasi alifanya maamuzi ya kuacha kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi wanaosababisha Ukimwi ARVs. Kwa mwezi mzima aliokuwa anaishi bila hizi dawa alikuwa na afya njema tu. Aliwashuhudia watu ukuu wa Mungu wake kwa uponyaji alioupokea. Hakwenda kuthibitisha kupona kwenye kituo cha afya kwa madai kuwa ana imani hana tena maambukizi.

Alitumia muda wake mwingi kutoa ushuhuda wa tiba ya kikombe kwa waliomzunguka na kwa mara ya kwanza maishani mwake alikuwa huru kutangaza rasmi kuwa alikuwa mwathirika kabla yakupoea uponyaji kwani mwanzo alifanya siri. Alikuwa ni chachu ya watu wengine wengi waliomzunguka na waliomsikia kushawishika kwenda Samunge kupata bidhaa. Alikuwa habari ya mji, alialikwa mpaka kwenye mikusanyiko ya kidini tofauti kutoa ushuhuda na kushawishi mamia wengine waliotilia shaka tiba ya Babu. Aliokoka rasmi na kuwa muumini wa kanisa fulani la kilokole na kati ya maagano aliyoyafanya ni kutumia afya aliyojaaliwa kueneza habari njema za Mungu (injili). Yote haya yalitokea ndani ya wiki sita tu tangu apate kikombe cha dawa ya babu.

TUMAINI NI BATILI

Ilimchukuwa Mama U miezi mitatu kuanza kudhoofu mwili kwa sababu ya kuacha kutumia ARVs. Marafiki wa karibu walimshauri kurudia dawa lakini Mama U aliwajibu kuwa anapitia majaribu na hatayumba kwani ana imani kuwa alipokea uponyaji. Alizishuhudia ndoto kadhaa alizoota wiki ya kwanza ya uponyaji zilizomthibitishia kupona. Alizishuhudia kwa kila aliyemtembelea na alizisimulia kwa watu kadhaa waliomshauri kurudia tiba ya hospitalini.

Miongoni mwa nukuu alizokaririwa akisema ilikuwa ni "Mtumishi Ayubu aliuliwa mifugo yake yote, mazao yake yote, watoto wake wote, akapata maradhi lakini aliendelea kumtumaini Bwana" . Aliendelea kukaidi ushauri wa wapendwa waliomzunguka na imani yake ilikuwa imara. Aligombana na rafiki zake wa karibu waliokuwa wanamhudumia anapozidiwa kwa sababu alikataa kunywa dawa.


TUMAINI BATILI LINAFIFIA

Alidhoofu kupita kiasi, mwili uliisha, macho yalipoteza nuru, ngozi iliunda makunyanzi na nywele zilibadilika rangi. Maradhi yaliambatana na kukata tamaa, hofu na hasira (pengine ni kwa sababu alihisi kudanganywa) kwani siku moja alimpiga rafiki yake aliyekwenda kumsaidia usafi nyumbani kwake akimtuhumu kumtangazia habari za kuugua kwake. Aliwapiga watoto wake akihisi wanamsema kwa watu na mtoto wake mmoja alitoroka nyumbani kukimbia kadhia inayoletwa na hali ya mama yake. Mwili wake ulishuka kinga na kuwa jamvi la mwaliko wa magonjwa yote nyemelezi (opportunistic diseases), mara maralia, mara kifua kikuu, mara kuhara.

Alishindwa kufanya kazi yake vyema, hivyo uchumi wake uliingia matatani na hata alipopata nguvu za kupika kwenye mgahawa wake watu waliogopa kwenda kwa sababu mbalimbali kama kinyaa, huruma na wengine walikuwa na imani kuwa upo uwezekano wa wao kupata maambukizi kwa kula chakula cha mwathirika. Washirika wake kibiashara walimkimbia kwani hali yake kiakili haikuwa rafiki wa wateja. Walienda kuendeleza shughuli mahala pengine. Alibaki peke yake, yeye na bidhaa ya tumaini alilouziwa kwa shilingi 500, bidhaa ya mazingaombwe iliyodumu kwa miezi kadhaa tu. Si tu afya yake ya mwili na akili vilikuwa rehani, ndoto zake za maisha, mipango yake na ustawi wa familia yake vyote vilikuwa kwenye ubao mdogo mbovu juu ya bahari iliyochafuka.

Mama U alifariki dunia miezi mitano toka asitishe matumizi ya ARV, kifo kilimkuta akiwa njiani akirudi Loliondo kujaribu kikombe kingine. Aliacha watoto watatu wakiwa bado wadogo sana na rasmi wakawa yatima kwani baba yao alifariki miaka kadhaa kabla yaMama U. Napata picha Mchungaji wa kanisa lake alisema "ni mipango ya Mungu", au "yeye alitoa na yeye ametwaa" na waumini walijibu "jina lake lihimidiwe".

Wakati Mama U akitangulia udongoni, Askofu aliendelea kuuza matumaini kwa waja wengine waliokata tamaa na Serikali ilimpa usaidizi kama kibali cha shughuli, kibali cha tiba na usaidizi kwenye miundombinu ya kiusalama, usafirishaji na huduma muhimu ili kuhakikisha bidhaa hii ya matumaini inawafikiwa na wengi na kwa haraka. Serikali ilithibitisha dawa haina madhara yeyote. Narudia DAWA HAINA MADHARA YEYOTE. Picha iliyokuwamo kwa wahusika serikalini ni KAMA HAIUI UKINYWA BASI NI SALAMA. Matokeo kando ya hii dawa kama hili la mama U halikuwa miongoni mwa shaka kuu la matumizi ya dawa hiyo.

NINI TUNAJIFUNZA?

Kabla ya hadithi ya kweli ya Mama U, Mwaka 2007, Mtanzania Emmanuel Didas alifanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu kwa kilichosemwa kuwa ni kuchanganywa kwa taarifa zake na mgonjwa mwingine Emmanuel Mgaya. Kufidia uzembe huu Taasisi inayojihusisha na masuala ya mifupa MOI kwenye hospitali ya muhimbili (waliopolazwa Emmanuel Didas na Mgaya) iliwapeleka wahanga wa tukio hili India kwa matibabu na kwa amri ya mahakama walikubali kulipa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa Didas aliyewashitaki MOI kwa madai (compesation for the injuries). Ripoti kadhaa zinasema uongozi wa Muhimbili uliwashughulikia wahusika kwa uzembe, sina shaka walisimamishwa kazi kwa muda au labda moja kwa moja au hata serikali kuwafutia leseni za udaktari.

Madaktari wana nguvu kubwa ya kuaminisha umma juu ya usalama na ufanisi wa dawa au taratibu za kimatibabu (medical procedures). Mara nyingi mtu yeyote mwenye haja ya tiba anachukua maoni ya kitabibu kutoka kwa daktari as literal and correct information. Haya mamlaka waliyonayo madaktari wanayo pia watabibu kando kama wachungaji, waganga wa jadi na wataalamu wa tiba za nyumbani (HOMEOPATHY) au hata wasoma nyota. Lakini linapokuja suala la kuwa accountable for malpractices Wachungaji wanaotuhumu kuponya hawaguswi. Mama U alikuwa ni alama moja tu kuwakilisha wengi waliofariki kwa kuacha matibabu rasmi ya kitaalamu yaliyothibitishwa kitaalamu.

National library of Medicine (NIH) wanaeleza kuwa makosa ya kidaktari (medical malpractice) ni kosa kisheria na ni kipengele mojawapo cha TORT. Labda kifo cha Mama U si TORT  kama tu yalivyo makosa yeyote ya kimatibabu yanayoweza kufunguliwa kesi za madai kama hiyo ya Emmanuel Didas. Je nani atawazungumzia waathirika wa madaktari wa tiba kando/mbadala na wafanyabiashara wa kuuza matumaini na kuwaomba kuthibitisha matumizi ya bidhaa zao kabla ya kuwapa watu? Na inahitajika watu wangapi kufariki kwa imani hizi ili iwe ni miongoni mwa mada kuu za mazungumzo kwa jamii na serikali na kuacha kuwa faragha?

Kuna haja gani ya wataalamu kuthibitisha dawa kama zimefikia kiwango cha ubora ambao serikali imejiwekea ikiwa wapo waganga wa jadi, wataalamu wa tiba za majumbani (HOMEOPATHY) na wachungaji wanaotoa hizi tiba bila kibali cha ubora na usalama kwa gharama za pesa, muda na maisha ya watu?

2 comments

  1. Mama U aliuziwa matumaini yaliyomponya kwa siku chache akaisahau tiba ya kweli.

    ReplyDelete