- Nina shaka na maana na kipimo cha ustaarabu kwa sababu kuu mbili. - Moja, uhalisia hauonyeshi hivyo, ni ngumu kujadili ustaarabu na kiumbe ambaye amemiliki na kuuza binadamu mwenzake kama bidhaa kitumwa, ametoa sadaka ya damu, amepigana vita kadhaa akigombea miliki ya ardhi, mipaka na rasilimali ambazo akifa anaziacha, anabagua haki ya umiliki wa rasilimali kwa kigezo cha jinsia na rangi, ukabila au utaifa na pia ngumu kujadili ustaarabu na kiumbe anayefuga majeshi kujilinda dhidi ya binadamu wenzake. Hizi na nyingine nyingi si dalili za kustaarabika.
- Pili, vyote (maana na kipimo cha ustaarabu) vimewekwa na yeye binadamu, kumjadili binadamu bila muktadha linganishi nje ya jamii yake. Labda ndiyo maana ustaarabu unapimwa kwenye kutendea usawa kwa binadamu tu na si viumbe wengine na mazingira (UBINAFSI). Kifupi kwenye mtihani, mtunzi ni binadamu, mfanyaji ni binadamu na msahihishaji ni yeye mwenyewe.
- Ufahamu: Uwezo wa kupokea na kutafsiri taarifa kwa muktadha na maana sahihi kiasi kuweza kufanya mrejesho stahiki.
- Mantiki: Uwezo wa kupangilia mawazo kwa uyakinifu wa kimaana na kimuktadha.
- Kutambua kuwa anaishi na kurindima na maisha, na kuhisi thamani ya uhai (being sentient).
- Kidole gumba kinachozunguka (Opposable thumb) kinachomuwezesha awe msanii, kiasi ameunda, umeumba, amechora, amejenga n.k.
- Lugha: Chombo cha kimapinduzi kinachomuwezesha kusafirisha taarifa haraka na kwa ufanisi wa hali ya juu).
SIMBA | BINADAMU |
Ana kasi ya kukimbiza windo | Hana kasi ya kukimbiza windo anatumia mitego, silaha na kulaghai (kufuga) |
Ana kucha za kurarua | Hana kucha za kurarua, anatumia nyenzo mfano kisu |
Ana machonge ya kuchana | Hana machonge ya kuchana, anatumia nyenzo |
Ana mataya yenye nguvu ya kutafuna nyama | Hana mataya yenye nguvu ya kutafuna, anaunguza na moto na mafuta/maji kwanza |
Mfumo wake wa kumeng'enya unaweza kumeng'enya nyama | Mfumo wake wa umeng'enyaji hauwezi kumeng'enya nyama mpaka iunguzwe |
Nyama ni chakula kikuu, hana mbadala wa chakula zaidi ya nyama | Nyama si chakula kikuu ni ziada |
Anawinda kwa ajili ya haja ya asili ambayo chakula tu | Anafuga kwa ajili ya haja za ziada kama ladha ya muda mfupi, na kuzalishia bidhaa kama mavazi na mikoba |
UTUMWA NA UFUGAJI
UTUMWA | UFUGAJI |
Binadamu ni bidhaa/mali/kizalisha mali | Mnyama ni bidhaa/mali/kizalisha mali |
Binadamu ananunulika/kuuzika kubadili umiliki (transfer of ownership) | Mnyama ananulika/kuuzika kubadili umiliki |
Hakuna thamani ya ndani ya mtumwa bali ile inayopimwa na nguvu yake ya uzalishaji/utimizaji wa haja ya mmiliki (no intrinsic value). Mfano: Binadamu ni bora akiwa anazalisha bidhaa, mrembo kumvutia mmiliki n.k | Hakuna thamani ya ndani bali ile inayopimwa na nguvu ya uzalishaji/utumizaji wa haja ya mmiliki (no intrinsic value). MFANO Ngómbe ni mzuri akiwa anazaa au kuzalisha, anatoa maziwa kwa ajili ya mfugaji n.k |
Hakuna marejesho/malipo kwa anayemilikiwa | Hakuna marejesho/malipo kwa anayemilikiwa |
Miaka bora ya anayemilikiwa (akiwa na nguvu na afya) ni miaka ya kumtumikia mmiliki Mf. binadamu mwenye nguvu, kijana, mrembo , mwenye kasi anamtolea hizi zawadi zote mmiliki na si kwa ajili yake | Miaka bora ya mnyama (akiwa na nguvu na afya) ni miaka ya kumtumikia mmiliki. mf. Ng'ombe akiwa na maziwa mengi si kwa ajili ya ndama wake bali ni kwa ajili ya mfugaji, akiwa na afya ni kwa ajili ya chakula cha mmiliki na si kwa ajili ya maisha yake |
Halali kidini na kijadi | Halali kidini na kijadi |
Haramu kisheria | Halali kisheria |
WAZO: ukiwa kwenye mtumbwi uliopotea baharini, yapo matunda, nyani mmoja, mbuzi mmoja na mtoto mdogo. Ukiwa kwenye hali ya kawaida kiakili utaanza kula matunda kisha mbuzi, kisha nyani alafu inapobidi kutimiza golden rule kuwa hakuna bora zaidi ya uhai wako utamla binadamu kwa mapambano. Nje ya hii order ni shaka la ufahamu.
Ipo nafasi sawa ya kupigania uhai kwa viumbe walao nyama?
Kiasili, kila kiumbe mla nyama ameundwa na nafasi sawa ya kupigania maisha. Ndio maana simba anaingia mawindoni kupambana na swala ambaye naye asili ilimuunda kujua na kukimbia hatari. Simba atapambana na atapata chakula kimoja kwa wakati mmoja, inaitwa fair chance to fight for survival na ipo kwa ALL SENTIENT BEINGS. hii ni sawa kwa chui, duma, mamba n.k isipokuwa binadamu. Binadamu ana njia zisizo za asili kupata chakula kwa sababu sio chakula chake cha asili. moja ya sadaka anazotoa ni kutotoa nafasi sawa kwa viumbe wahanga kupigania maisha yao akiamua kuwafuga, kuwategea mitego au gesi za sumu si nafasi sawa ya kupigania uhai. Kama binadamu ana akili ya kuunda vifaa haimaanishi ana uhuru wa kutumia vifaa hivyo kuumiza. MWONEVU.
WAZO 2: Maluweluwe ni kusema virutubisho muhimu vinapatikana kwenye wanyama tu. Ni binadamu tu anashinda kwenye viwanja vya mazoezi kupunguza mwili, ni binadamu tu anasumbuka na Obesity (unene kupita kawaida) na ni binadamu tu anayeumwa magonjwa ya moyo. Kiasilia kundi la primates wote ni wala mimea, kama Orangutani, Bonobo, chimpanzii n.k ni wanyama wa karibu na binadamu kibaiolojia, kifiziolojia na kianatomia, binadamu hawezi kusimama nao hata kidogo kwa nguvu, kasi au ustahimilivu dhidi ya kiu, njaa na maradhi na ni wala mimea. Labda tuwaulize mamalia wakubwa zaidi mwituni Tembo na Kifaru wanapata wapi virutubisho ikiwa wao pia ni wala mimea? Virutubisho ni sababu ya UONGO.
Mungu kaumba wanyama kuliwa na binadamu?
Mungu (anayeshuhudiwa na binadamu) aliumba wanyama waliwao kama chakula akawapa milango ya fahamu, neva za maumivu, hofu na haja kuu ya kuishi. Rudia hiyo sentensi iliyopita tena. Mnyama anapochinjwa anasikia maumivu kwakuwa ameumbiwa vihisi maumivu, anasikia dhuruma kwakuwa ameumbiwa haja ya kuishi na anasikia hofu kwakuwa pia ameumbiwa wasiwasi. Mungu wa huruma na upendo kwa binadamu tu, alishusha kitabu cha uongozi kwa binadamu tu kuruhusu matumizi ya wanyama kama chakula. Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, hizi ni busara za vitabu vinavyosemwa ni vitakatifu na vina elimu na busara zisizo na kipimo.
WAZO 3: Basi nami nakuja na Kitabu cha Mungu wangu, Mungu wa wanyama, Mungu anaitwa ASILI, dini inaitwa MANTIKI na dhambi pekee ni kuwa MJINGA.
Ni Mungu yupi ambaye hajajua daraja la juu zaidi la ustaarabu,upendo na huruma?
Kupenda, kuheshimu na kulinda binadamu ni daraja la ustaarabu, Kupenda, kuheshimu na kulinda wanyama ni daraja la juu zaidi la kustaarabika. Binadamu wastaarabu hawajajua daraja hili, Lakini cha ajabu ni kwamba hata nguvu kuu ya imani zao (MUNGU) naye hajajua daraja hili la juu la kustaarabika. Kama ambavyo tumesubiri miaka na miaka Utumwa na biashara yake kutangazwa ni haramu, basi tusubiri miaka mingine mingi biashara ya kitumwa ya wanyama iwe haramu. AU TUSUBIRI MPAKA SIKU WANYAMA WAONGEE KUWA WANAONEWA NDIO TUAMINI?
WAZO 4: Unahitaii Mungu kusema jambo ni baya ili liwe baya? Na je, jambo ni baya kwa sababu mungu kasema au ni baya ndiyo maana mungu kasema?
Binadamu ni wa maalumu kuliko viumbe wengine?
Kujua umuhimu na umaalumu wa kitu ni kupima changamoto kipindi hakipo. Hii ni mifano ya kimantiki ya yatayotokea ikiwa binadamu atatoweka. Joto litapungua kwa sababu hewa ya kabonidioksaidi itapungua. Hewa hii inazuia joto kuondoka duniani. Binadamu anazalisha zaidi hewa hii kwa kuunguza ghafi za kaboni na visukuku(fossils) kwa shughuli mbalimbali binafsi, Ozoni itafunga kabisa kwa sababu inapata mushkeli kwa uzalishaji wa hewa chafu unaotokana na shughuli za kibinadamu, Uzalishaji wa chupa za plastiki utaisha, kelele za viwanda na vyombo moto zitaisha, Uharibifu wa mazingira kwa sababu ya vita na shughuli nyingine kama uchimbaji madini, kilimo na ujenzi utaisha. Udongo utasheheni rutuba, kifupi dunia itapona vidonda.
Umuhimu wa binadamu upo wapi? Ikiwa Phytoplanktoni inazalisha karibia asilimia 70 ya oksijeni duniani, Nyuki ambao ni wachavushaji wa karibia theluthi moja ya mimea inayomea ardhini kwa njia hiyo kuzuia dunia nzima kuwa jangwa? Minyoo midogo ya udongoni wanaendesha mzunguko wa rutuba udongoni? viumbe ambao wakiondoka sio tu binadamu atakufa bali hata dunia itatikisika.
Umaalumu wa binadamu upo wapi? ikiwa ameundwa na vijenzi vile vile vilivyounda sehemu kubwa kama si yote ya ulimwengu, Haidrojeni, Oksijeni, kaboni na Naitrojeni. Namtuhumu binadamu UJIVUNI wakati vipo asivyoviweza, asivyovijua na vipo muhimu na maalumu zaidi yake.
Kama ni maalumu kwa sababu ya uwezo wa kuongea, kuwasiliana, kujenga n.k basi tai ni maalumu kwa sababu anaona mbali, kinyonga ni maalumu kwa sababu anaweza kunakiri rangi za mazingira akinuia kujificha, popo ni muhimu analala akining'inia kichwa chini miguu juu, ndege anapaa, samaki wanapumua kwenye maji. Umaalumu unapotea ikiwa kila mtu ana kipawa chake.
Je kufuga na kula ni vyema kwa sababu imehalalishwa kisheria?
Being legal, does not mean moral all the time. Kitu kuwa halali haimaanishi ni adilifu. Miaka kadhaa nyuma utumwa ulikuwa ni halali, ukeketaji wa mabinti ulikuwa ni halali na mpaka sasa binti analipiwa mahari akibadilishiwa mji wa mwanaume kutoka kwa baba kwenda kwa mume, haina maana ni adilifu. Kuweka sheria zinazohalalisha ubazazi ni sababu tu ya UBINAFSI.
JE,BADO BINADAMU NI MSTAARABU?
Kuwa mstaarabu ndio uongee ustaarabu, acha kuuza binadamu wenzio, ndio uongee ustaarabu, acha kukandamiza wanawake, watoto, maalbino na walemavu wengine ndio uongee kuhusu ustaarabu. Acha kubagua umiliki wa rasilimali kwa kigezo cha rangi na jinsia ndio uongee kuhusu ustaarabu, acha kulipia au kukubali malipo ya mahari na kukeketa wanawake ndio uongee ustaarabu. Linda mazingira , acha kupigania mipaka ya kuchorwa kwenye karatasi ndio uongee kuhusu ustaarabu. Acha kuwagawia watoto makabila na dini, concepts zinazoishi vichwani zikiwagawa kiasi kuchukiana na mwisho, acha kuonea wanyama ndio tuongee kuhusu ustaarabu. Kwa yeyote ambaye ataona picha hizi mbili chini ni tofauti basi hayuko tayari kuanza safari ya kustaarabika. Kwa niaba ya wanyama wote, Nawasilisha!
Dhambi pekee ni kuwa mjinga
ReplyDelete