Utangulizi
Nakumbuka wakati fulani tulikuwa tunatazama runinga na familia, maudhui mbalimbali yalirushwa hewani, wasaa ukaenda tukiyatazama na kati ya hayo yakawemo yaliyohusu kampeni ya kushawishi wanafunzi wa jinsia KE kuchagua michepuo ya Sayansi kwenye masomo. Mnadi wa suala hilo ambaye sikumbuki jina lake alikuwa ni mmoja wa watumishi wa serikali alikuwa anatoa ahadi ya kuwepo kwa mipango madhubuti ya kuwasaidia mabinti kufanikiwa kwenye masomo hayo iwapo wataamua kuyachagua. Alinadi mpango huo akiwia kushawishi kina dada wachague michepuo hiyo. Bibi yangu ambaye akiwa ni miongoni mwa wanafamilia kwenye kilinge kile alitoa kauli ambayo ndiyo iliyochochea mimi kuandaa makala hii, nakuu ”Nyakati hizi ni nyakati bora kwa wanawake kuliko nyakati zote zilizopita”.
Kati ya mazungumzo yalijishikiza kwenye kauli ile yalizunguka taarifa kuwa ilikuwa ngumu kiasi gani miaka ya zamani kwa binti sio tu kuwa na uhuru wa kuchagua nini cha kusoma bali hata kuwepo shuleni tu. Mazungumzo yalifikia kwenye masuala mbalimbali ya kijamii kuwazungunguka kina dada. Alizungumza kuhusu ukandamizaji na unyanyasaji wa kijinsia na hali ya mabinti kutokuwa sehemu ya taswira ya kesho ya maendeleo ya jamii. Maswali mengi yalizalishwa na mjadala huo kichwani mwangu, maswali kama, hali hiyo ilikuwa kwa jamii yake tu kwakuwa alihusisha ukandamizaji ule na upotovu wa baadhi ya mila na desturi za kabila lake, maswali kama, nini kilifanyika kuleta mabadiliko tuyaonayo sasa.
Miaka kadhaa mbele nikiwa na utimamu wa kutosha, mazungumzo yale yalinirejea na nikaamua kuchukua jukumu la kufuatilia ili tu kujibu baadhi kama sio maswali yote yaliyonitatiza ili tu kujiridhisha. Nikiwa kwenye usukununu wangu kusaka maarifa, nilishangazwa kwa namna ambavyo, sehemu nyingi za ulimwengu kama sio zote zilitawaliwa na hii stigma dhidi ya wanawake. Nilishangazwa na muendelezo wa kipindi kirefu cha wanawake kuwa kwenye wingu zito la mifumo kandamizi. Jamii nyingi hazikuwapa wanawake uwakilishi wa kutosha kwenye masuala ya utawala, walinyimwa haki ya kupiga kura na kushiriki kikamilifu kwenye maamuzi ya kijamii na kiuchumi. Hawakuwa na haki ya kumiliki rasilimali, kupata ajira au kujitegemea kiuchumi. Baadhi ya jamii hasa za Kiafrika zilikuwa na mila na desturi hatarishi kwa afya ya mwili, akili na hisia kwa kina dada kama ukeketaji, ndoa za lazima na za utotoni. Hawakuwa na mamlaka juu ya miili yao wala maamuzi kwenye masuala ya uzazi kiasi kuzalishwa watoto wengi bila mapumziko na mara nyingi walikuwa ni wahanga wakuu wa ukatili wa majumbani (Domestic violence). Pia kuna nyakati lilizuka wimbi la ubakaji na mauaji kiasi ilikuwa ni hatari kwa wanawake hata tu kutembea barabarani wakiwa peke yao. Ila zaidi nilishangwazwa na juhudi za wakereketwa na wadau mbalimbali wakiongozwa na wanawake wenyewe kwa vipindi tofauti kuhakikisha kurasa hii nyeusi inafunikwa na tukiwa kwenye milenia mpya, kuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha mafanikio ya juhudi zilizofanywa na wanaharakati na wakereketwa wa haki za wanawake kuwakomboa kina dada kutoka kwenye mazingira na mifumo kandamizi.
Migomo baridi, maandamano, usambazaji wa elimu kuhusu masuala ya jinsia, uundaji wa sera za nchi na irani za vyama vya kisiasa na vyama vya wafanyakazi kusimamia usawa wa kijinsia na kubwa zaidi kuanzishwa kwa taasisi mbalimbali za umma na binafsi zilizojikita katika masuala yanayomhusu mwanamke katika nyanja mbalimbali zilikuwa ni sehemu tu za mapambano makubwa kuielekea dunia mpya ya wanawake na nikaelewa kwanini bibi alisema kauli ile kuhusu wakati huu kuwa wakati bora kwa kina dada.
Kati ya mwaka 1960 na 2020, Tanzania ilishuhudia kuanzishwa kwa taasisi nyingi za kuwasaidia, kuwakomboa na kuwatetea wanawake dhidi ya changamoto mbalimbali zinazowakabili, mfano Idara ya Ustawi wa Jamii chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto; Taasisi ya Wanawake ya SAWA; Kanzidata ya Wanawake na Uongozi Tanzania (TWL), Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA); Taasisi ya Wezesha Foundation inayojihusisha na uwezeshaji wa vijana na wanawake; pamoja na Umoja wa Kamati ya Wanawake wa THTU Taifa. Pia zipo taasisi za kimataifa zenye uwakilishi nchini kama Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN-Women) na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF).
Chama kikongwe cha TANU na baadaye CCM, kwa nyakati tofauti, kiliwahi kujumuisha Sera ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto kama sehemu ya mipango yao ya maendeleo. Haya ni matunda ya kazi ya pamoja ya wadau, wanaharakati na wakereketwa waliodhamiria kuleta mabadiliko ya kweli kuelekea dunia mpya yenye usawa wa kijinsia.
Ni muhimu kutambua wanaume walihusika kwa kiasi kikubwa katika harakati hizi, wakishiriki katika uundaji wa maono, mipango na utekelezaji wa mikakati ya mabadiliko kwenye masuala ya kijinsia.
Mnamo tarehe 10 Januari 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alianzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuitenganisha kutoka kwenye iliyokuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 57A na 57B la tarehe 24 Januari 2022, wizara hii ilipewa jukumu la kuratibu na kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto, Wazee na Makundi Maalum; kwa ajilii ya kuratibu usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali; ili kuendeleza usawa wa kijinsia na kusimamia juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia. Uundwaji wa wizara hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa masuala ya wanawake yanapata msukumo wa kiutendaji na kiutawala. Nimeonyesha hiyo mifano kuonyesha juhudi za kumkwamua mtoto wa kike kwenye matatizo mbalimbali.
Men In Nutshell
Wakati nikitafakari kauli ya Bibi kuhusu wakati huu kuwa wakati bora kwa wanawake, fikra kuwa upi ni wakati bora kwa wanaume zilianza kuniwinda. Niliwaza kama kuna wakati bora zaidi kwa wanaume kwenye historia ya maisha ya binadamu kwenye uso wa dunia. Kwa sababu ya uhaba wa majadiliano kuhusu hili wazo kuhusu jinsia ya kiume, ilinibidi kuangalia kwa namna tofauti. Namna mojawapo ilikuwa ni kuangalia nini ni matatizo yanayoikumba jinsia ya kiume (exclusively) kwa ujumla wao. Nikawaza kuyatambua matatizo ya sasa na kulinganisha na yale ya miaka iliyopita au hata ya kale.
Tazama baadhi ya takwimu hizi za miaka ya karibuni.
- Rekodi za Shirika la Mpango wa Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-habitat) za mwaka 2024 zinasema, wakati idadi ya watu wanaoishi mitaani bila makazi (homeless) imefikia milioni 150, watu zaidi ya bilioni 1 hawana mahali stahiki walau pa hali ya chini kibinadamu kuishi na asilimia 60 kati yao ni wanaume. Idadi hii ni ya nchi 75 tu kati ya zote 195 zilizokuwa na taarifa rasmi za uwepo wa watu wasio na makazi. Ikimaanisha nchi 120 hazina taarifa rasmi kuhusu hali hii.
- Hadi mwaka 2021, zaidi ya asilimia 70 ya jumla ya waathirika wa madawa ya kulevya walikuwa ni wanaume.
- UNODC ililipoti kuwa hadi mwaka 2019 watu zaidi ya milioni 11 walifungwa jela kwa vifungo vya kati na maisha, kati yao wafungwa wa idadi sawa na asilimia 93 walikuwa ni wanaume.
- Jinsia ya kiume inaongoza kwa idadi ya vifo vya ajali, ulevi na uhalifu.
- Jinsia ya kiume inaongoza kwa idadi kwenye masuala ya vifo vinavyotokana na vita na machafuko ya kisiasa na kitaifa
- Shirika la kimataifa la masuala ya kazi ILO linaripoti kuwa, angalau wanaume 51 kati ya 100,000 hufariki kwa vifo vinavyotokana na kazi zao (workplace fatality), na sababu zikiwemo ajali kazini, madhara ya kemikali na uchovu wa jumla. Idadi hiyo ikilinganishwa na watu 17 kati ya 100000 tu kwa upande wa wanawake. Hii inatoa taswira ya tabia ya kufanya kazi za hatari kwa sababu ya malipo mazuri, au uhaba wa ajira nyingine za kawaida, ukubwa wa majukumu ya kifamilia na kiu ya kufanikiwa mapema.
- Idadi ya vifo vinavyotokana na kujiua kwa sababu ya msongo wa mawazo ni mara mbili kwa wanaume dhidi ya idadi ya wanawake kwa wastani kwa ripoti za hadi mwaka 2015
- Ripoti zinasema, wanaume hushuka kimaisha kwa asilimia kati ya 10 hadi 40 baada ya talaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ile ya malipo ya malezi ya watoto.
Kwakuwa baadhi ya takwimu nilizoziainisha hapo juu, ni za miaka hii ya milenia mpya unaweza kudhani kuwa hapo kale mambo yalikuwa nafuu, La hasha, umri wa kuishi kwa wanaume haukuwahi kuwa bora mwanzo kuliko sasa, kazi hatarishi zilikuwepo hapo kale na mazingira mabaya vibaruani hayajawahi kuwa imara hapo kale kuliko sasa, mategemeo kutoka kwenye jamii yake hayajawahi kuwa nafuu sasa kuliko hapo kale, afya ya akili haijawahi kuwa bora sasa kuliko hapo kale, upweke na sonona havikuwa bora hapo mwanzo kulinganisha na sasa. Yote yapo na yemekuwa maradufu.
Miaka hiyo hiyo ambayo jinsia KE walikuwa kwenye nyakati mbaya ndiyo hiyo miaka ambayo Jinsia ME walipigana vita ya kwanza na ya pili, walifanya kazi ngumu bila nyenzo nzuri kwa sababu ya uduni wa teknolojia, walipambana na sonona na magonjwa ya akili bila kuwepo kwa mifumo saidizi kama tiba au ushauri wa kitalamu. Jambo kuu ambalo hasa ndio dhima kuu ya hili andiko ni kuwa, ni jinsia moja tu walichukua jukumu la kutambua kuwa hali wanazopitia ni matatizo. Na jinsia hiyo sio wanaume.
Kwa muktadha wa kiujumla, jamii haina huruma sana na jinsia ya kiume, labda kwa sababu ya kuona kuwa wanaume ni wahanga wa matatizo wanayoyatengeneza wenyewe hivyo kuhisi wanastahili au kuhisi wanaweza kuyavumilia au kuyamudu. Lakini inashangaza kuona kuwa wanaume hawana muda wa kujiangalia wao wenyewe kwa ujumla wao kukata mizizi ya matatizo yanayowaathiri na zaidi kuwa watazamaji, kama sio washiriki wa yanayoendelea.
Ni kawaida kuona mwanaume akiwa anaomba barabarani kwa miaka mingi, bila msaada, akiwa anatembea uchi kwa sababu ya matatizo ya akili kwa miaka mingi bila msaada, akiwa anateketea kwa madawa ya kulevya na ulevi bila msaada. Wapita njia watapita na kuona haya masuala na kuendelea na shughuli utadhani hakuna cha ajabu kilichotokea. Ni nadra kuona wanawake hawana makazi, wanaomba barabarani, wanaokota makopo au wapo mitaani kwa sababu ya matatizo ya akili. Matatizo haya kwa wanawake hayaonekani kirahisi sio kwa sababu wao hawayapati matatizo ila ni kwa sababu wanawake wana ashki ya kujisimamia wenyewe. Ashki iliyorithiwa na jamii, wakiwemo wanaume.
Misaada mingi ya matatizo yanayoathiri exclusively jinsia ya kiume huwa ni binafsi, ila hakuna jitihada za jumla kusaidia mizizi ya matatizo yanayowakumba wanaume kwa ujumla, jambo ambalo ni la kushangaza ni kugundua kuwa wanaume wapo kwenye nafasi za kufanya hivyo na hutumia nafasi hizi kusaidia wanawake. Hakuna taasisi za kiserikali au binafsi kuangalia matatizo yanayoathiri jinsia hii kwa ujumla au kama zipo basi sio rasmi. Kifupi ni kuwa hakuna harakati rasmi zilizoanzishwa kwa ajili ya kuangalia matatizo yao.
Sanaa ya Kujikata Mguu
Licha ya kutokuwepo kwa juhudi za pamoja za kusaidia wanaume, tatizo la kudidimia kwa ustawi wa jumla wa jinsia ME, lipo kwa wanaume wenyewe. Wanaume wanashiriki kwenye mizizi ya matatizo haya kama vyanzo au kama waendelezaji wa mnyororo wa matokeo.
Kuelewa changamoto hii ni muhimu kuelewa huu mtazamo wa hali halisi ya mahusiano kati ya mwanaume na mwanaume kijamii. Kwa mwanaume kuwa thabiti na shupavu kwenye dunia hii ni suala lisilo na mjadala na ushupavu huu ni kwa sababu washindani wake ni shupavu pia. Washindani ambao pia ni wanaume. Mwanaume hushindana na mwanaume mwingine. Hushindana kupata kazi nzuri, makazi mazuri, mke mzuri, wateja wengi, rasilimali nyingi n.k.
Ni asili ya ulimwengu sio tu huu wa milenia mpya bali hata miaka tele iliyopita, mwanaume hawezi kudanganya njiani kuelekea mafanikio bali ni lazima awashinde wanaume wengine shupavu. Wachache waliodanganya huanguka haraka, kufa mapema au kujiweka kwenye matatizo na mikono ya sheria. Ushindani huu wa asili ulipaswa kutosha kumuumiza mwanaume ila ukosefu wa mifumo ya misaada kwa wanaoanguka ndio changamoto kubwa na cha zaidi mwanaume kuwa sehemu ya udidimizwaji wa ustawi wa jinsia hii adhimu.
Tafakuri
- Mwanaume anaweza kuua mwanaume mwenzie kwa sababu ya ajira au mgao wa pesa
- Mwanaume anaweza kuua mwanaume mwenzie kwa sababu ya mapenzi.
- Mwanaume anaweza kumsitiri mwanamke aliyerukwa akili barabarani ghafla ila anaweza kumwacha mwanaume kichaa anayetembea barabarani uchi kwa miaka mingi.
- Mwanaume anaweza kupiga mwizi wa kiume mpaka akafariki na kumpeleka polisi mwanamke aliyemuibia au hata kumsamehe.
- Mwanaume atamsifia mwanamke kwa kuwa mstaarabu, msafi au mpole kusema hizi ndio sifa nzuri kwa binti, ila mwanaume atamsema mwanaume mwenzake akisema sifa kama usafi, ustaarabu au nidhamu, kwa madai kuwa ni ushamba.
- Mwanaume hugandamiza tabia njema kama kutokunywa pombe na kuvuta bangi, kutokuwa malaya, kutocheza kamari au kutoendesha vyombo vya moto kwa kasi ni kama ni udhaifu.
- Mwanaume anamcheka mwanaume mwingine akiwa na huzuni kiasi kulia kwa sababu kulia ni udhaifu..
- Mwanaume anamnunulia mwanaume mwingine vilevi na kuchukua sifa kwa kumlewesha ila anamnunulia mwanamke gari au nyumba.
- Mwanaume ndiye anayemuuzia mwanaume mwingine madawa ya kulevya.
- Mwanaume ndiye anayeua mwanaume mwingine kwenye vita.
Kwa nchi yangu, ambayo wanaume wametawala kwenye vitengo nyeti vya kiserikali, huwa sehemu za utekelezaji wa sera zinazosaidia kina dada kujikwamua kijamii, kiuchumi na kiafya ila hawajawahi kuwaza kuhusu kusaidia wanaume ni jambo la kujitafakari sana.
Sijawahi kuona wala kusikia walau hata waomba kura wanaweka suala la kusaidia jinsia ya kiume kujikwamua kwenye matatizo mbalimbali kama sehemu ya maono kwenye uongozi wao ujao. Wala hutasikia matatizo ya jinsia hii kuwa sehemu za sera za chama au serikali. Walau asilimia 60 ya uongozi serikalini ni wanaume, Walau asilimia 60 ya watunga sheria bungeni ni wanaume, inakuwaje hakuna walau mazungumzo kuhusu matatizo yanayoathiri hii jinsia exclusively kama ilivyo kwa wanawake? Na hii ndio maana ya kujipiga risasi wenyewe mguuni kwa sababu wanaume tupo kwenye nguvu ya kufanya mabadiliko chanya ila tunashiriki kwenye kudidimiza ustawi.
Kwanini Mwanaume asaidiwe?
Nilikuwa nasikiliza shuhuda mbalimbali za watu waliochukua maamuzi ya kukimbia nchi na kwenda ughaibuni kutafuta maisha, asilimia 99.99 za mashuhuda walikuwa ni wanaume. Shuhuda zao zinaumiza hisia sana kwani hutawaliwa na changamoto zisizofikirika, wengi hugeuka kuwa watu wabaya, wezi, wazurumaji au wauaji na yote hayo ili tu dunia izunguke wakiwa hai. Wengi hufa njiani au hufia wakiwa huko bila kufikia uwanda wa majani mabichi wanayoyaota, na baadhi wanaoishi mpaka sasa bado maisha yao hayana dira.
Nikawaza kwanini sijawahi kusikia walau mwanamke mmoja kufikia uamuzi huu mgumu na hatari wa kukimbia nchi kinyemela na kwenda kujaribu maisha mahala pengine? Nikagundua wanawake huwa na machaguzi kadhaa nafuu kabla ya kufikia kwenye hatua hii ya kukata tamaa. Machaguzi mfano uwepo wa vikundi, taasisi au wizara zinazoweza kusaidia kina mama waliokata tamaa au kuishi kwenye mazingira hatarishi. Machaguo ambayo wanaume hawana. Mwanaume aliyefikia hatua ya juu ya Desperation ni mwanaume hatari, hudhuru au kujidhuru akikosa mwangaza au mwongozo. Matokeo ya hawa waliokata tamaa ni vikundi kama Wapiga nondo Mbeya, Mbwa mwitu na Panya rodi Dar es salaam, wachoma visu Arusha au wezi wa kutumia silaha tunaowasikia kila mara. Mwanaume ni kioo cha taifa, udhaifu wa kundi kubwa la wanaume ni udhaifu wa taifa.
Tanzania ikiwa na umri wa miaka zaidi ya 6o, imeshuhudia maraisi 5 wa Kiume, bila kuwepo kwa mifumo ya usaidizi, kuwaangalia wanaume wenye changamoto za kimaisha, kimwili, kiakili na kihisia. Lakini, Ilimchukua Rais Samia Suluhu miezi kadhaa tu tangu kuingia madarakani kukaimu nafasi ya Marehemu Dr Magufuli kuanzisha wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu, tarehe 10 Januari, 2022 baada ya kuitenganisha kutoka iliyokuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Ukitazama majukumu ya wizara hii mpya utagundua yalilenga kuwatazama wanawake kwa ukaribu zaidi ili kuwasaidia kutatua changamoto zao. Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali na 57A na 57B la tarehe 24 Januari 2022, Majukumu ya Wizara hii yalijumuisha: Maendeleo na utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wanawake, Wazee, Watoto na Makundi Maalum. Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Ukuzaji wa usawa wa Kijinsia, Kutokomeza ukatili wa Kijinsia, Uratibu wa Mashirika ya Kimataifa chini ya sekta hii.
Nilijisikia wivu kuona kiongozi mkubwa wa serikali anatumia fursa na nafasi aliyokuwa nayo kufanya mabadiliko chanya kwa watu wa jinsia yake huku jinsia nyenzie tukiendelea kuficha moto kwa viganja.
Hivi karibuni Wachezaji wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania Twiga Stars wameanzisha jumuiya yao kutambuana na kutafuta namna ya kusaidiana kujikwamua baada ya kustaafu kucheza soka. Sina shaka miaka kadhaa mbele hawatakuwa kwenye maisha duni, sio kwamba muunganiko wao utaleta pesa za ghafla bali kuungana pamoja kuna tija kwani wanaweza kusaidika kirahisi. Tayari wameanzisha Bonanza la kila jumamosi kukutana kucheza na kusimamia wachezaji wachanga wa kike kujifunza namna ulimwengu wa soka unavyoenda. Wamejiweka kwenye nafasi ya kupokea wadhamini na hatua hii itawasaidia kujikwamua kwenye changamoto mbalimbali baada ya kustaafu, yote haya yatakuwa ni kwa sababu ya juhudi za wakereketwa waliowiwa kufanya mageuzi kwa jinsia hii.
Hitimisho
Nina haja ya kushawishi wanaume wenyewe kusaidiana kwenye changamoto kabla ya kufikia hatua za kufanya maamuzi mabaya au maamuzi magumu. Ziwepo juhudi mbalimbali za kusaidia wanaume kwa makundi kwa ajili ya kujinasua kwenye wingu hili kabla ya kuanguka. Uanzishwaji wa vikundi vya majadiliano kujadili masuala yanayoathiri jinsia hii kwa kina inaweza kuwa mwanzo mzuri kabla ya hatua ya taasisi za kijamii na za masuala ya afya na kiuchumi.




Siku zote hamna ninachojutia uwepo wako Kaka vina umesimama nasisi katika sanaa zote na kutuongezea maarifa ya msingi big up man
Nimesoma walaka huu nimejikuta akili yangu inafunguka na kuanza kujifikilia kama mwanaume,, ujue tulio wengi hatujifikilii wenyewe isipokuwa tunafikilia kuusu familia yaani wake na watoto wetu kiufupi hatujali nin kitatupata ila itakuwaje kwa familia kama nisipo fany jambo mimi.
Nakala hii ime provoke mind yangu walau kwa asilimia kubwa kutambuwa kwanini life expectancy ya jinsia ME ni fupi.. sisi wenyewe hatujajijengea uwanja au viwanja (option) tafauti tofauti kabla ya hatujachukuw hatua ngumu au kuchagua chaguo hatari kwa maisha yetu.. we fight for our life to live lakini ndo tunaishia kwenye kuchagua hatua ngumu zinazohatarisha maisha yetu.
I wish hili andiko liende viral, maybe hata hizi taasisi za kusaidia jinsia KE zitapungukiwa majukumu. Imagine kama asili mia kubwa ya kibaka, wezi, wabakaji, watelekezaji wa familia ni wanaume.. na u imagine kungekuwa na taasisi zinazosaidia boys. I hope matukio yangupungua na hizi kesi za kila siku za ustawi wa jamii zingepungua..
Nimewaza pengine wanajaribu ku solve shida sehem pengine hazipo
Black maradona🔥
Black maradona🔥🔥
Kwanza waraka huu kwangu mimi nilivokuwa nasoma naziona kabisa ngoma zako ulizotoa zinazomuhusu mwanaume👊, wanaume tunayopitia kwenye maisha yetu inaonekana kama tunastahili tupitie hayo na imekuwa kawaida tu ila kama vitatokea hivo unavyoongelea kaka basi mwanaume atafanya mengi na kwa ukubwa zaidi kwenye jamii ambayo mwanaume ni kioo.
Nakusifu sana Dizasta kwa uandishi huu makini. Umeeleza vizuri tatizo kwa kutoa vyanzo vya taarifa.
Wazo langu, naona kama matatizo mengi, kama si yote, yanayomkumba mwanaume ni matatizo yanayoikumba jamii kwa ujumla bila kujali jinsia. Japo ni sahihi kwamba yanaathiri jinsia ya kiume zaidi ya jinsia ya kike. Pili, jinsia pinzani( ya kike) si chanzo kikubwa cha haya matatizo yanayowaathiri wanaume zaidi. Angalia upande wa pili utagundua kilio chao ilikuwa ni kuhusu matatizo waliyosababishiwa na jinsia ya kiume. Mfano, wakati wanawake hawana uhuru wa uchaguzi kuhusu miili yao, hii ilikuwa ni sababu wanaume waliamua hivyo, ndio maana sikushangaa kuona juhudi zilizofanyika na pande zote za jinsia kuyatatua. Mwanaume atakufa sababu ya vita, maradhi au ajali kwenye mazingira hatari ya kazi si sababu ni matokeo ya maamuzi ya mwanamke, bali ni matokeo ya hali au maamuzi ya jamii nzima.
Hii inafanya niwaze kwamba wito wa kumkomboa mwanaume ni sawa na wito wa kuikomboa jamii nzima. Na ninafikiri watu hawajawahi kuacha kupigana hii vita. Faida pekee ninayowaza ya kufanya hili pambano kuwa sawa na pambano la kuwaokoa wanaume ni kwamba inaweza kuchochea utambuzi utakaopelekea kupunguza baadhi ya vyanzo vya tatizo, hivyo kuleta ushindi mapema. Kwa mfano, mwanaume akitambua kwamba anapowaalika wanaume wenzake kwenda vitani kuua wanaume wengine itasababisha vifo vingi vya wanaume wenzake, anaweza kuwaza vyema wakati mwingine. Je hii sio sawa na kusema kuanzisha vita kunasababisha vifo vingi vya watu wenzetu? Ambayo ni bora zaidi?
Kwa kifupi, nafikiria ni bora zaidi ingekuwa kuhusu watu na si kuhusu jinsia fulani ya watu.
Asante kwa mjadala!
Ukombozi wa fikra💯✔️
Naiona nafasi ya kujifunza vitu vingi na kufanya vitu vingi juu ya hii makala, kwa chochote kilichoelezwa Mimi ni wa pili baada ya dizasta, kwa sababu kwenye cycle yangu ninao watu wengi ambao wamekua adicted na hili janga, natamani kusimulia yote itakua makala nayo
Vina sijawahi kukupinga
Nilishawahi kuwaza kwanini wanaume hatupewi kipaumbele kwenye mambo mengi … Tushalishwa sera hii toka swala la women empowerment ilipoanzishwa beijing 1990’s …
Na swala la kuanzisha hii kampeni ya men empowerment inapaswa ianzie kwenye familia kwanza …maana mwanaume anadharaulika sana endapo akiwa hana uchumi mzuri
Kihombo
Ni Leo tu nimeingia lakini madini haya ni muhimu Sana na yako na faida Kwa mwanaume.
Duuh shida kubwa sometimes ni kwamba wanaume na jamii tunaamini na kuhisi kwamba hizi changamoto zimewekwa kwa ajili yetu hivo hatufungui akili zetu kama wanaume kujisaidia.Ila shout out to u BLACK MARADONA
Saluti broo ngoma zaidi ya kio na vyo jiona
👏👏👏
Mwenyezi Mungu ashukuriwe sana, tuna kila namna ya kujivunia uandishi wako Sanaa inayoweza kufikirisha kwa mapana ikiwa ndani ya fikra chanya
Kwa elimu Mungu akulinde nasi elimu itufungue na kutusaidia maishani