Mwaka 2024 umepita, Kwa hitaji la wengi nimeandaa list yenye baadhi ya Albums nilizosikiliza, vitabu nilivyosoma, makala nilizosoma na filamu nilizoangalia kwa mwaka huu wote.
VITABU
Mwaka huu nilisoma vitabu vitatu na hii ndio review yangu kwa ufupi kwa kila kimoja.
- Ujamaa – Essay on Socialism – The late Julius K. Nyerere
Kitabu kilichapichwa kwa mara ya kwanza mwaka 1961, na kufanyiwa marejeo mara kadhaa na baadaye kutafsiriwa kwa lugha ya kiingereza mwaka 1968. Nilikisoma kwa mara ya kwanza mwaka 2013 lakini nikawiwa kurudia sasa nikiamini uwezo wa kuelewa maudhui yake kwa mapana umekua. Kwenye nakala hii Hayati Julius K. Nyerere alijadili maono yake ya kuwepo kwa aina maalumu ya ujamaa inayoendana kwa asilimia mia moja na tamaduni, mira na desturi, aina ya itikadi, kiwango cha uelimikaji na mtindo wa maisha wa nchi za kiafirka (hasa Tanzania). Wazo la aina hii ya ujamaa lilitumika kama sera kuu ya chama cha siasa cha TANU ambacho Mwalimu alikuwa ni mmoja wa waasisi na mwenyekiti wake wa kwanza. Mwandishi alielezea mafanikio na changamoto za wazo hili hasa kwenye uhalisi wa utekelezaji. Nakala hii ilibaki kumbukumbu ya juhudi za mwanzo za kumkomboa mwananchi masikini baada ya Ukoloni. Hili andiko lilisanifisha kanuni muhimu zilizosimamia haki na usawa kama zilivyojadiliwa kwenye azimio la Arusha. Nukuu yangu pendwa kutoka kwenye nakala hii ni ile iliyomnukuu mwalimu kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii kwa ustawi wa familia zetu, akisema “Mgeni siku mbili;siku ya tatu mpe jembe”.
- The moral Lanscape – How science can determine human values – Sam Harris
Binadamu wa karne ya 21 wamekuwa karibu kama wanaishi kijiji kimoja kwa sababu ya kukua kwa teknolojia hasa kwenye eneo la mawasiliano, uchukuzi na usafirishaji. Ukuaji huu umefanya dunia kuwa ndogo. Binadamu wanajijamiisha kwa karibu na kwa haraka zaidi bila kujali maeneo waliyopo. Hii imekuza umuhimu wa mazungumzo kuhusu falsafa ya maadili wakati wa kujijamiisha. Mwandishi wa The Moral Landscape, Kitabu kilichochapishwa mwaka 2010, Sam Harris anajadili wazo la kuhusianisha maadili na ustawi wa maisha ya binadamu (Well-being) akisema mijadala ya maadili haitakuwa na maana kama haitahusisha ustawi wa maisha ya binadamu na wanyama. Pia alijadili kwa kiasi gani sayansi itaweza kutupa kweli ya nini maana ya ustawi hasa kwenye eneo la afya ya akili, mwili na hisia za binadamu na viumbe. Pia alijadili tamaduni na imani mbalimbali zinavyoweza kuhatarisha afya ya mwili, akili na hisia, lakini pia afya ya uchumi wa binadamu. Nukuu yangu pendwa kutoka kwenye kitabu hiki ni “Wanawake na wanaume walio kwenye hukumu za kunyongwa, wapo pale kwa sababu ya mchanganyiko wa malezi mabaya, mawazo na itikadi mbaya, imani mbaya, vinasaba mbaya au bahati mbaya”
- Who we wrestle with God – Jordan Peterson
Kitabu hiki kilichapishwa November 2024, Ndio kilikuwa kitabu cha mwisho kusoma mwaka huu. Mwandishi anajadili hadithi mbalimbali za kale za kifasihi na umuhimu wake kwenye mustakabali wa maisha ya sasa. Mwandishi anaamini kuwa fasihi za zamani ni muhimu kwa sababu zinatupa picha ya mtindo wa kufikiri wa jamii za kale. Mwandishi pia anajadili dhana ya ukaidi, sadaka, mateso na ushindi kwa kutumia hadithi mbalimbali za kibiblia. Jordan anachagua Biblia kuelezea maudhui yake akiamini ni kitabu stahiki zaidi kiushawishi, kiumri na kiasilia. Moja ya subject matter alizojadili mwandishi ni IMANI na kujitoa SADAKA. Anasema dunia na mapana yake ni kubwa sana kiasi hatuwezi kuimaliza kuielewa hivyo kwenye maisha mafupi ya binadamu huwa tunachagua vile tunaavyoona ni muhimu. Na hapo ndio Imani na sadaka vinapokuja kwani kuchagua ni kuamini kuwa upo sawa na machaguo yako na sadaka za kuacha vingine (choices and cost of opportunites). Mfano wa hadithi alizotumia kujadili maudhui ni ile hadithi ya Yona aliyeikimbia sauti ya Mungu iliyomtuma kwenda Nineveh kueneza habari njema, Yona alikaidi na mwishowe kumezwa na samaki. Mwandishi alihusisha hii hadithi na athari za kukimbia majukumu kwa nafasi uliyopewa. Nukuu yangu pendwa kwenye kitabu hiki ni “kanuni mbaya zikienziwa, wafalme wabaya wakisimamishwa na maadili mabaya yakiwekwa na watu, ni watu wenyewe ndio wataangamia”.
FILAMU
Nilipata wasaa wa kuangalia filamu kadhaa mwaka 2024 na hizi ni 5 zilizonivutia zaidi.
1. 12 angry men – 1957
Baraza la waamuzi 12 walipewa jukumu na mamlaka ya kuamua kesi ya kijana aliyetuhumiwa kumuua mzazi wake. Kesi iliyoonekana ni ya dakika kadhaa tu kwa sababu ya nguvu ya ushahidi uliowekwa ila ikageuka kuwa shughuli ya kichunguzi. Waamuzi 11 waliamini kuwa mtuhumiwa ni mkosefu na anastahili adhabu wakati mmoja akiwa na shaka na aina ya ushahidi ulioletwa, hivyo kuwa na jukumu kuwashawishi waamuzi wenzake kujadili upya ushahidi ili kuondoa shaka. Filamu hii ya seti moja ila ilikuwa na uwezo wa kuambukiza shauku muda wote kwa sababu ya ubora wa mazungumzo na muendelezo wa matukio. Moja ya nukuu niliyoipenda kwenye Filamu hii ni “Kama unataka kupiga kura kuwa fulani ana hatia, sema kwa sababu una uhakika ana hatia na sio kwa sababu umechoka kusikiliza shauri”.
2. Schindller’s list -1993
Filamu ya wasifu wa kweli inayomuhusu Oskar Schindler, Mfanyabiashara mwenye tamaa ya pesa aliyeingiwa na ubinadamu kiasi kugeuza kiwanda chake kuwa kimbilio la wahanga wa serikali ya ki-nazi ya Ujerumani. Filamu hii iliandaliwa kuenzi mchango wa Oskar kwenye mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, itikadi kali ya utaifa, udikteta na ukatili wa serikali ya Adolf Hitler..
3. Enemy – 2013
Filamu ya saikolojia inayomuhusu mhadhiri wa chuo kikuu anayeingia kwenye mkanganyiko na mwigiza filamu anayefanana naye kwa asilimia 100. Baada ya kuambiwa na rafiki yake kuwa amefanana na mwigiza filamu huyo anaenda kuangalia filamu zake na kuzalisha kiu ya kumjua, kiu inayoishia kumuweka kwenye njiapanda inayozaa matatizo makubwa. Filamu inayojadili umuhimu wa kurekebisha mazoea mabaya kabla hayajawa tabia. Mazoea kwenye filamu yanawakilishwa na buibui mdogo anayeonyeshwa mwanzo wa filamu kisha kuwa mkubwa mwisho wa filamu.
4. The Assasionation of JESSE JAMES by the Coward ROBERT FORD – 2007
Mja mwoga Robert Ford anategemea kulakiwa kishujaa na jamii yake baada ya kumuua jambazi anayeogopwa kwenye mji wake. Kiu ya umaarufu na heshima inamfanya kubadili jina kisha kuandika kitabu kusheherekea mauaji yake mwenyewe lakini bado jambazi Jesse anaimbwa kama shujaa huku yeye akiwa hatambuliki kabisa. Hasira inampanda baada ya filamu kutengenezwa kumuenzi Jesse. Robert anajaribu kuishi lakini uhalisia kuwa watu hawamwoni kama shujaa unamtafuna. Kiu yake ya kuheshimiwa inarudi na mwishowe inamwingiza kwenye kifo.
5. Cosmos: A Spacetime Odyssey, Season 1
Msimu wa kwanza wa mfululizo wa sukununu ya binadamu kuhusu ulimwengu na elimu ya anga. Chaneli ya National Geographic wanaungana na Mkufunzi wa masuala ya astrofizikia Neil de Grease Tyson kubadili kitabu kuwa onyesho la televisheni.
Nilisikiza album kadhaa kwa minajiri ya burudani na elimu na hizi ndizo zilizonivutia zaidi:
- The auditorium Vol 1 by Common & Pete Rock
- Knock Madness by Marcus Hopsin
- Mapinduzi halisi by Professor Jay
- Extiction level Event 1 by Busta Rhymes
- Extiction level Event 2 by Busta Rhymes
- Mhadhiri by Maalim Nash
- Mitaa flani by Songa
- In my room by Jacob Collier
- Dawn by Yebba



